Kwa mujibu wa wabunge hao ambao walitaka majina yao yasitiriwe kwa sasa, baadhi ya wasanii hao ambao wengi ni mastaa wamekuwa wakiwazukia na kuwapiga mizinga jambo linalowashangaza hasa wakizingatia kuwa, wapiga mizinga hao wana majina makubwa na huonekana wakitembelea magari ya kifahari.
“Hivi nyie mapaparazi, mnashindwa kabisa kukomesha hii tabia ya mastaa wa Bongo Muvi? Hawa jamaa ni ombaomba sana.
“Wamekuwa wakitupiga mizinga sana. Tunawashangaa maana wengine wana majina makubwa, wanatembelea magari ya kifahari lakini bado wanaomba pesa ndogo,” alisema mbunge mmoja ambaye anatoka kwenye moja ya majimbo ya Mkoa wa Dar es Salaam.
KINACHOWASHANGAZA WABUNGE
Kwa mujibu wa wabunge hao, linalowashangaza zaidi ni kwamba wasanii hao ambao ni wake kwa waume, wamekuwa wakipiga mizinga ya pesa ndogo badala ya kuomba pesa za kufanyia mambo makubwa yenye mikakati mizito.
“Mtu anakuja, anasema anasumbuliwa na kodi ya nyumba au anasema hajala. Hivi kweli mastaa wakubwa kama akina…(anataja jina) ni wa kuomba vijisenti kama vya kodi ya nyumba jamani?” alihoji mbunge mwingine kati ya watano waliokuwa wakizungumza na gazeti hili.
Waheshimiwa hao waliendelea kuwaanika mastaa hao kwa kudai kwamba, walichogundua ni kuwa inapotokea wakapewa hitaji lao la fedha, huishia kukaa baa hadi usiku wa manane na asubuhi wakiamka wako vilevile kama hawakupewa.
MWAKIFWAMBA ABANWA NA RISASI
Ili kuweka sawa madai hayo mazito na yenye aibu kubwa kwa tasnia hiyo maarufu nchini, Risasi Jumamosi lilimtafuta Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania ‘TAFF’, Simon Mwakifwamba ambaye alikiri kuwepo kwa malalamiko hayo ya wasanii wake kuwa ombaomba!
HUYU HAPA MWAKIFWAMBA
“Ni kweli kabisa. Mimi mwenyewe nimewahi kusikia malalamiko hayo, lakini unajua tena ni mambo binafsi, mtu anapiga mizinga kwa mambo binafsi si rahisi kumwingilia,” alisema rais huyo.
Aliendelea kusema kuwa, katika vikao mbalimbali vya kisanii, amewahi kuweka wazi msimamo wa taasisi kwamba kila msanii aishi maisha yenye heshima huku akiwa mbali na mazingira yenye kusababisha aibu katika jamii.
KUMBE HATA JK ALIWAHI KUMLALAMIKIA
Katika kuonesha hasira zake juu ya tuhuma hizo zenye dharau katika gemu la filamu, Mwakifwamba alikwenda mbele zaidi kwa kusema kuwa, katika moja ya mazungumzo yake na Rais wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Kikwete ‘JK’ aliwahi kumlalamikia kwamba, wapo mastaa ambao kazi yao ni kupiga mizinga isiyo na tija.
“Rais mwenyewe aliwahi kuniambia kuna wasanii wakiwasiliana na yeye wanamwambia mambo ya pesa za kula.
“Kuna msanii aliwahi kumtumia meseji JK akimwambia, ‘mjukuu wako leo hali mbaya’,” alisema Mwakifwamba.
Akaendelea: “Sasa we’ unakutana na rais badala ya kumweleza mikakati mikubwa na nini cha kusaidiwa kuifanya tasnia iweze kuendelea, unapiga mizinga hujala, ni aibu sana.”
WALISHAMPIGA ‘MIZINGA’ HADI ‘MTOTO WA MKULIMA’
Mwakifwamba hakukubali kufumba midomo yake bila kupasua yote ambapo alizidi kudai kuwa, hawashangai sana wasanii wake hao kwani waliwahi kumpiga mizinga hadi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda ‘Mtoto wa Mkulima’.
“Niliwahi kukutana na Waziri Mkuu Pinda, nikamwomba mambo ya kuisaidia tasnia ya filamu Tanzania, akasema afadhali mimi nimeongea vitu vya maana, kuna wenzangu alikutana nao ‘wakambomu’ fedha za matumizi binafsi, nilishangaa sana,” alisema Mwakifwamba.
RISASI LAWASAKA MASTAA, WAPATIKANA HAWA:
Jacqueline Wolper, ni staa wa filamu za Kibongo. Filamu yake ya kwanza ni Ama Zao Ama Zangu. Yeye alipoulizwa kuhusu madai hayo, alisema:
“Ni kweli, sikatai kwamba hiyo tabia ipo tena sana tu. Lakini wanaoongoza ni mastaa wa kiume, hao ndiyo wanaotutia aibu ya kuonekana sisi ni o
mbaomba.”
STEVE NYERERE
Yeye ndiye Mwenyekiti wa Bongo Movie Unity. Alisema anavyojua kuna kuonana kirafiki na waheshimiwa na kuonana kiajenda.
“Tabia ya kuomba fedha kwa waheshimiwa ipo. Lakini linapokuja suala la tasnia yetu kupeleka hoja kwao, tunaanza hoja baada ya hapo kuna waheshimiwa wengi wana urafiki na wasanii, tunaitana pembeni na kupiga kirungu.
“Siwezi kukaa na waheshimiwa kama Rostam Aziz, William Ngeleja, Mheshimiwa Abood na Nimrod Mkono halafu nikawaacha hivihivi, kisa eti mimi ni Mwenyekiti wa Bongo Muvi,” alisema Steve akionesha kumshangaa mwandishi aliyempigia simu kutaka usawa wa mizani ya habari hiyo.
ODAMA YEYE
Jennifer Kyaka ‘Odama’ yeye alipata umaarufu mkubwa kupitia Tamthiliya ya Odama iliyokuwa ikirushwa na Televisheni ya Taifa (wakati huo TVT). Alipopigiwa simu iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa licha ya kurudiwa mara kadhaa.
AUNT EZEKIEL
Risasi pia lilimtafuta nyota mwingine aliye mahiri kwenye sinema za Bongo, Aunt Ezekiel ambaye filamu iliyompaisha sana inaitwa Miss Tanzania. Yeye simu yake ya mkononi ilionesha kutokuwa hata na laini kwa wakati huo.
RAY AFUNGUKA
Staa mkongwe katika gemu tangu enzi za Kaole Sanaa Group, Vincent Kigosi ‘Ray’ aliposakwa na kuulizwa kuhusu madai hayo ya wasanii kuwa ombaomba alisema:
“Wasanii wengi wanawaza maisha ya hapa na si baadaye. Badala ya mtu kuweka shida zake kwenye mfuko wa karatasi, anaweka kwenye rambo ambao unapiga kelele.
“Mwisho wa siku anaomba shilingi milioni tatu akagombolee gari au asaidiwe kodi ya nyumba, anasahau kuwa kapata nafasi ya kuonana na mheshimiwa azungumzie tasnia tunavyonyonywa hadi kuuza hati miliki,” alisem Ray.
No comments:
Post a Comment