Stori: Sifael Paul
Lile
sakata la kukamatwa kwa yule mganga wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu
Abdul ‘Diamond Platnumz’, Ustadh Yahya kwa msala wa wizi wa gari,
limechukua sura mpya baada ya mke wa mwenye gari, Edric Magayane kuibuka
na kufunguka mazito.
Akizungumza na gazeti hili, mke huyo aliyejitambulisha kwa jina la
Emida Denson alisema kuwa gari hilo aina ya Toyota Rav4 lilikuwa mali ya
familia kabla ya mumewe kudai lilipata ajali hivyo lipo gereji.
Alisema kuwa baadaye mumewe alidai kuwa aliliuza akaongezea fedha kisha akanunua lingine aina ya Toyota Prado.
Alisema habari kuwa gari hilo liliibwa maeneo ya Kariakoo-Msimbazi,
Dar hazikuwa za kweli kwani ukweli ni kwamba mumewe huyo alikuwa
amemhonga mwanamke aliyemtaja kwa jina moja la Mwanahamis.
“Huyo
Mwanahamis amenisababishia mateso makubwa kwenye ndoa yangu karibia
miaka miwili sasa. Yaani ndoa yangu ni sarakasi tupu kwa sababu yake.
“Ukweli ni kwamba baada ya kuhongwa lile gari alikuwa hajui
kuliendesha. Alichokifanya akamwachia Ustadh. Hayo mengine ya
kushirikiana juu ya biashara zao za uganga hayanihusu.
“Sasa basi baada ya kuona gari liko mikononi mwa Ustadh ndipo mume wangu akalitaka ndiyo maana wamefikia hapo.
“Kinachoniuma ni kwamba mbali na gari, mume wangu alifikia hatua ya
kuja kumpangishia Mwanahamis jirani na nyumba yetu maeneo ya
Machimbo-Mwisho wa Lami (Yombo jijini Dar)
“Mbaya zaidi watu wakawa wanamuona mume wangu akiingia kwa Mwanahamis, nimedhalilika sana.
“Nalea watoto wanne peke yangu, wakwangu wawili na wawili wa mume wangu kwa mwanamke mwingine.
“Baada ya kuona ndoa inanitesa nilikwenda kwa mchungaji Kimaro
aliyefungisha ndoa yetu kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT), Usharika wa Kariakoo nikamweleza mateso ninayopata.
“Alituita wote, akasemwa lakini baada ya hapo manyanyaso yakaendelea japo walihamia Banana-Ukonga ndiko wanakoishi hadi leo.
“Pia nilikwenda kwenye Dawati la Jinsia wilayani Temeke na baadaye Ustawi wa Jamii.
“Huko kote ilishindikana na sasa bora anipe talaka yangu tugawane mali
kwa sababu nilipokutana naye hakuwa na kitu chochote, tulikuwa tukilala
chini,” alisema mwanamke huyo kwa uchungu huku akitoa cheti cha ndoa
(nakala ipo).
Kwa upande wake mume wa mwanamke alipotafutwa na kusomewa mlolongo wa
sarakasi alizozieleza mkewe, alisema kuwa gari hilo lilikuwa mali yake
na kwamba lilipata ajali likakaa gereji muda mrefu na lilipopona alikuwa
akilitumia mwenyewe.
Kuhusu kuwa na hawara Mwanahamis, jamaa huyo alidai kwamba aliamua
kuwa na mwanamke huyo kwa kuwa mkewe alikuwa ana matatizo ambayo hata
hivyo hakutaka kuyaainisha.
“Naishi naye (mkewe) lakini kila mtu na
chumba chake, huyo mwanamke ana matatizo yake ndiyo maana nikatafuta mtu
mwingine, hizo habari anazolalamika, anazusha tu, nimempa uhuru aniache
na wangu na yeye atafute mwanaume mwingine,” alisema mwanaume huyo.
Kuhusu gari analodaiwa kukutwa nalo mganga wa Diamond, habari zilieleza
kuwa Ustadh aliachiwa kwa dhamana na bado gari hilo lipo mikononi mwa
polisi likisubiri kesi kwenda mahakamani.
No comments:
Post a Comment