Biashara ya dawa za kulevya inaonekana kushamiri nchini, huku kukiwa na maswali mengi juu ya akina nani hasa wahusika wa shughuli hii, hata inashindwa kukomeshwa.
Waliopewa mamlaka kuzuia dawa hizo nao wanahusika au hawana ujuzi, wafukuzwe?
Baadhi ya wananchi waliozungumza na mwandishi wa
makala hii, wana mashaka kwamba huenda baadhi ya vigogo au wafanyakazi
waliopewa mamlaka kupambana na dawa nchini, wanahusika kufanya biashara
hii au kuwasaidia wanaoifanya kwa manufaa yao, madai ambayo wamekuwa
wakiyakanusha vikali.
Hata hivyo baadhi ya watu ambao wamewahi kuwa
majambazi na kujihusisha na biashara haramu, akiwamo mchungaji mmoja
kutoka Arusha ambaye amewahi kuwa jambazi kabla ya kuamua kuokoka na
kumtumikia Mungu, anasema ni vigumu mno na huenda ni jambo
lisilowezekana kufanikiwa kufanya mambo mabaya nchini kama ya ujambazi
au dawa za kulevya na ukadumu katika kazi hiyo kama hauna mtandao na
wale ambao wanahusika katika kuzuia vitendo hivyo.
“Kama una mawasiliano na wenye mamlaka utafanya
biashara yoyote chafu, kama huna ni ngumu kutokamatwa, mimi nimewahi
kuwa jambazi, ninaongea haya kwa uzoefu, sio kweli kwamba ulinzi nchini
ni mbaya, bali kuna watumishi si waaminifu” anasema Mchungaji huyo.
Kwa uzoefu wake ni kuwa iko haja kwa viongozi
walioko Serikalini kama kweli wana lengo la kupambana na dawa za
kulevya, kwanza kuwachukulia hatua wote ambao waliwakagua na kuwaruhusu
wahusika wa dawa wanaokamatwa kupita.
Ni kama hakuna lengo la kupambana na dawa za kulevya
“Kama mtu amepita uwanja wa ndege, inapaswa
kujulikana alikaguliwa na nani? Wote waliohusika wakamatwe mara moja,
waunganishwe kwenye kesi ya hizo dawa za kulevya, hii itaonyesha kweli
Tanzania tuna lengo la kupambana na dawa za kulevya, lakini
kinachofanyika sasa ni usanii wa mchana kweupe,” anasema Mchungaji huyo
ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini.
Hatua kali kwa wauza dawa
Baadhi ya wananchi akiwamo Ameria Haule, mkazi wa Ubungo anashauri kutungwe sheria kali za kupambana na dawa za kulevya.
Aidha, Juma Hamisi wa Mtongaji, na Tuma Msongwa wa
Manzese, Dar es Salaam wanasema pale ambapo mtu amekamatwa na aina
yoyote ile ya dawa za kulevya, na kukawa na uthibitisho, kusiwe na haja
ya kufanya upelelezi juu yake zaidi, badala yake hukumu itolewe mara
moja. Hali kadhalika wakashauri dhamana iondolewe, wakisemabiashara hii
ni sawa na mauaji.
Kituo cha daladala kwa Manyanya
Mojawapo ya vituo vya daladala ambavyo vinadaiwa kutumiwa kwa
dawa za kulevya ni cha daladala cha Kinondoni kwa Manyanya, kama
unaelekea Posta ukitokea Kinondoni.
“Ni kawaida kuwaona vijana wakisinzia hapa kuanzia
asubuhi hadi asubuhi, kama kweli wenye mamlaka wana lengo la kupambana
na dawa, wangekuja hapa ikawasomba hawa wote wanaosinzia, kisha
ikawapime ili kuona walicholewa kimetokana na nini…kuna madai kuwa hao
ndio wauzaji wazuri wa rejareja hapa Kinondoni, hali kama hiyo iko pia
vituo vingine vingi vya daladala, huenda ndio sababu kwanini inakuwa
vigumu kupiga marufuku wapiga debe kuwepo, maana wauza dawa
wanajichanganya na wapiga debe,” anasema mkazi mmoja wa eneo hilo ambaye
aliomba jina lake lisiandikwe gazetini.
Ubungo darajani
Katika maeneo ya Ubungo kuna watu kadhaa
wanahusika na dawa hizi; Kwa mfano yuko jamaa ambaye huzunguka usiku
akisambaza dawa za kulevya kwa gari lake dogo. Hali ni mbaya zaidi eneo
la Ubungo Maziwa, wapo hadi akina mama kadhaa kwenye vijiwe vya vijana
wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Maeneo mengine ya Tanzania
Karibu nchi nzima, kuna kashfa hii ya kuwapo kwa
dawa za kulevya, huku maswali makuu yakielekezwa kwa wana usalama nchini
kama ni kweli hawaoni yanayoendelea.
Iundwe tume ya siri
Baadhi ya wananchi wanashauri kuundwe kikosi cha
siri kuchunguza utendaji wa askari ili kutoa mashaka ambayo yanaonekana
kuongezeka miongoni kwa jamii kuwa baadhi yao huenda wanashiriki katika
biashara hii ya dawa mbalimbali za kulevya yakiwemo cocaine, mirungi na
bangi.
Wanahoji ni kwanini Serikali ni kama inaonekana
kushikwa na kigugumizi katika kupambana na tatizo hili la dawa za
kulevya, licha ya idadi ya watumiaji ikionekana kuongezeka kadri siku
zinavyokwenda mbele.
Wengine wakashauri Rais Kikwete kumaanisha katika
kuchukua hatua na kuwachukulia hatua viongozi ambao wanaonekana wazi
kutochukua hatua
Ahadi nyingi vitendo haba
Licha ya kuwapo madai mengi miezi ya hivi karibuni
ikiwemo kwamba kuna viongozi wa dini wanahusika na dawa za kulevya,
wapo wabunge waliosema wanawajua wenye kufanya biashara hiyo, baadhi ya
viongozi wakielezwa kuhusika.
Hali ya dawa za kulevya nchini
Kwa mujibu wa ripoti ya ofisi ya Waziri mkuu, Tume
ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya, tatizo la dawa za kulevya
nchini limeendelea kukua licha ya jitihada mbalimbali zinazofanyika
katika kupambana nalo.
Hali hii inadhihirishwa na kiasi kikubwa cha dawa
za kulevya kilichokamatwa hususan heroin na cocaine katika mwaka 2011
ikilinganishwa na mwaka 2012.
Takwimu zinaonyesha kuwa kilo 264.3 za heroin
zilikamatwa mwaka 2011 ikilinganishwa na kilo 185.8 zilizokamatwa mwaka
2010. Takwimu hizi zinaonyesha.
Ongezeko la asilimia 42 la kiasi cha heroin
kilichokamatwa katika kipindi cha mwaka mmoja tu. Aidha, mwaka 2011 kilo
126 za cocaine zilikamatwa ikilinganishwa na kilo 63 zilizokamatwa
mwaka 2010 ambalo ni ongezeko la asilimia 100.
No comments:
Post a Comment