Studio hii iliyopo maeneo ya ‘uswahili’ imezingirwa na nyumba nyingi kiasi cha kushindwa kuijua njia kwa uharaka zaidi pale mtu anapotaka kufika kwa prodyuza huyo. Studio hii ni ndogo yenye vifaa vichache tu vya kimuziki lakini yenye prodyuza makini na mwenye kipaji.
Shadrack Willced Mongi maarufu ‘Sheddy Clever’ ndiye prodyuza wa studio hii iliyotengeneza wimbo wa ‘My Number One’ unaomilikiwa na mwanamuziki Naseeb Abdul ‘Diamond’, wimbo uliofanya vizuri katika levo za kimataifa.
Hata hivyo sehemu ya mahojiano na mwandishi wa Starehe ni kama ifuatavyo;
Swali: Mbona Studio yako ipo uchochoroni hivi?
Jibu: Unasema uchochoroni! Wasanii wengi wamekuja hapa na wanatumia muda mwingi kuwepo ndani ya studio hii huku wakitumia vyakula vya hukuhuku kwetu uswahili, si jambo la ajabu. Lakini ni mazoea tu kwetu tunaona sawa na kwa upande wangu inanipa hamasa kwani najisikia huru kufanya kazi nikiwa maeneo haya.
Swali: Ndiyo kusema Diamond alikuja kurekodi kwenye studio hii?
Jibu: Ndiyo alikuja kurekodi katika studio hii na alikuwa akikaa hapa kutwa nzima. Yule jamaa anafanya kazi sijawahi ona kutoka kwa wasanii wengine akija hapa anatumia muda mwingi kujenga mashairi, hata hivyo anatumia akili kubwa sana katika kufanya kazi si sawa na vile watu wanamwona. Korasi ya wimbo wa My Number One tulitumia zaidi ya saa 12 kuitengeneza na saa nyingine 12 kuirekebisha, yupo makini sana. Ilichukua miezi sita kukamilika.
Swali: Ilikuwaje akapajua hapa?
Jibu: Diamond alinitafuta yeye mwenyewe, ilikuwa saa mbili asubuhi akanipigia na kunifahamisha jina lake akasema anakuja, kwa kuwa namba niliyokuwa nayo alishaacha kuitumia nilidhani si yeye lakini baada ya muda nikashangaa amefika. Alinitaka nimsikilizishe midundo nami nilifanya hivyo hatimaye akapenda mmoja wapo, basi tulipeana mikakati kazi ikafanyika.
Swali: Kazi uliyoifanya imeweza kumwingizia kitita kikubwa cha pesa mwanamuziki huyo vipi kwa upande wako inakuneemesha vipi?
Jibu: Hapana nilimfanyia kazi akanilipa ujira wangu mzuri tu, hivyo huko mbele ni kazi yake. Lakini katika upande wa hatimiliki hivi sasa tupo mbioni kuhakikisha chama chetu cha maprodyuza cha Tanzania TSPA kinasajiliwa ili kuweza kutetea kazi zetu na hatimiliki.
Swali: Umechukua hatua gani kwa prodyuza aliyechukua biti ya wimbo wako na kuichakachua kwa kutengeneza kazi feki?
Jibu: Huyo mtu namtafuta sana tena sana, sijapata tu mahala anapofanyia kazi.
Swali: Tuambie uhalisia wa kazi zako ulianzia wapi?
Jibu: Nilianza mwaka 2005, nikiwa mkoani Tabora katika studio za rafiki zangu. Lakini studio yangu ya kwanza ilikuwa ni pale Student Center kulikuwa na mzungu mmoja aliitwa Father Clombi ndiye aliyekuwa mmiliki. Nikiwa huko nimepata kutengeneza vibao kadhaa vilivyofanya vizuri katika redio mbalimbali mkoani hapo. Niliamua kuondoka huko mwaka 2008 wakati huo nilikuwa nimeshapata jina kidogo. Nilifika jijini na kuanzisha studio pale Liwiti. Mtu aliyenisaidia sana ni Mbishi Real na kunipa uzoefu mkubwa katika kazi hii baadaye nikahama na kufika hapa Da West.
Swali: Kazi yako ya kwanza kabisa kuitoa na ikafanya vizuri ilikuwa ipi?
Jibu: Nivute Kwako wa Dayna aliyomshirikisha Barnabas. Wimbo huu ulinitambulisha katika ramani ya muziki wa kizazi kipya, tangu hapo walianza kumiminika wasanii maarufu wakitaka niwatengenezee kazi.
Swali: Ni kazi zipi maarufu ulishawahi kuzifanya?
Jibu: My Number One wa Diamond, Marry Me wa Rich Mavoko, Zilipendwa wa Matonya, Yatakwisha wa Ben Pol ft Linah, Mtoto Amekuwa wa Pasha, Swaga wa PNC na Ney wa Mitego na nyingine nyingi tu.
Swali: Una mikakati ya kuhama eneo hili na vipi kuhusu vifaa vya kisasa?
Jibu: Ninamalizia kujenga nyumba yangu huko Kinyerezi, hivyo nikimaliza tu studio yangu itakuwa nyumbani kwangu na huko ndiko nitafunga vifaa vya kisasa tofauti na hapa.
Swali: Unafanya shughuli gani tofauti na kazi yako ya utayarishaji wa muziki? Umepata faida gani kutokana na kazi yako?
Jibu: Mimi ni mjasiriamali nina duka linalouza CD, nina banda linaloendesha shughuli za michezo ya tv kwa watoto, bodaboda na vinginevyo. Nimeweza kujenga nyumba yangu mwenyewe, namiliki gari langu binafsi, nimekuwa na marafiki wengi na kujuana na watu mashuhuri kupitia kazi yangu.
-Mwananchi
No comments:
Post a Comment