POOL PARTY

POOL PARTY

Tuesday, June 18, 2013

MAISHA FEKI YA MASTAA WENGI WA BONGO


TASNIA ya muziki wa kizazi kipya Bongo kwa sasa imeshika kasi, wasanii kwa kiasi kikubwa wameweza kuwekeza na hata majina yao yamekuwa juu kiasi cha kujijengea imani kubwa mbele ya jamii.
Imani hii kubwa na ushabiki uliokithiri, imezua jambo jingine kubwa ambalo limekuwa tatizo la kimaendeleo. Tatizo hilo ni wasanii kujikuta wakiendeshwa na umaarufu wa majina yao katika namna ya wanavyoishi.
Imebainika kwa kuwa majina yao ni makubwa kuliko uwezo wao wa kuishi. Jambo hili limewafanya wasanii hao waishi maisha feki mbele ya jamii yao.
Kwa kuishi maisha hayo, wamejikuta wakitumia gharama kubwa katika kuishi maisha ambayo si ya daraja lao.
Mavazi
Ukianzia na mavazi, kwa kuwa tu anajulikana yeye ni yule msanii aliyeimba wimbo fulani maarufu, basi hata kama hana mavazi ya gharama atajitahidi hata kwenda kuazima, ili mradi mashabiki wake wakimwona wamkute nadhifu.
Awali tabia hiyo ilidhaniwa ni ya wasanii wa dansi pekee hasa Wakongomani, lakini sasa ni fasheni kwenye Bongofleva.
Inakubalika na ni dhahiri unadhifu kwa watu wenye mvuto kwa jamii ni jambo lililo wazi, lakini unadhifu unahusiana vipi na gharama?
Wengi wanapotelea hapa, wanafikiri unadhifu ni kuvaa vitu vyenye gharama kumbe uchaguzi wa vitu vya kawaida na mpangilio vinaweza kukufanya kuwa nadhifu kuliko vitu ghali.
Angalia mavazi ya Michael Jackson, yalikuwa ya gharama sana lakini si kweli kwamba mavazi yale ndiyo yalikuwa yakisababisha aonekane nadhifu kuliko wasanii wote duniani, alikuwa tu ni Mfalme wa Pop.
Lakini Bongo ukiachilia mbali kuazimana, kuvaliana na kuambukizana magonjwa, kuna kundi kubwa la wasanii ambao hupenda kujihusisha na maduka ya nguo ili mradi tu wapate kupendeza.
Usafiri
Ukishakuwa staa, tayari kuitwaitwa barabarani, kufuatwa na watoto ukiwa katika matembezi yako, ama kuombwa kupiga picha na mashabiki wako na mambo mengineyo kama hayo ni jambo la kawaida.
Wasanii wetu wanahisi hii ni ghasia na kuwakimbia mashabiki wao. Huukimbia kabisa usafiri wa umma, yaani daladala au wakati wanaenda mikoani huona bora hata wakodi magari badala ya kupanda basi.
Kuna asilimia kubwa ya wasanii tunaowaona wanaendesha magari kana kwamba wanayamiliki, kumbe si yao. Wengi huyakodi ili wakionana na mashabiki wao angalau waonekane wao ni wa matawi ya juu.
Jina linaendelea kuwa kubwa huku mhusika akiteseka kwa kuingia madeni makubwa.
Amini usiamini humu ndimo asilimia kubwa ya kipato cha msanii wa kizazi kipya kinapopotea. Magari hukodishwa kuanzia Dola 25 mpaka Dola 40 kwa siku kulingana na aina ya gari.
Makazi
Hapa ndipo ambapo hawajali kabisa, wengi wao huishi kwa kutegemea wazazi na wengine huishi kwenye nyumba za kupanga kwa kuchangia au kukaa tu kwa mtu huku wakiamini ipo siku mambo yatakuwa sawa wajenge.
Nyumba wanazoishi wengi wao ukiangalia na mavazi wanayovaa na magari wanayoendesha ni vitu tofauti. Wengi huweka kipaumbele mwonekano wa nje kuliko hata wanapoweka ubavu.
Ni wasanii wachache wanaomudu maisha yao kutokana na kipato kilivyo.
Ukiangalia mavazi, usafiri na huku anataka kuonekana kila sehemu ya starehe, sehemu ya pato hupotea huko na mwisho wa siku hubakia kuwa na umaarufu wa maneno na sifa za mdomoni .
Biashara?
Wengi zimewashinda kutokana na ukweli kwamba hawana uzoefu na tija katika biashara. Huanzisha miradi kwa kasi kwa kushirikiana na watu, lakini huwa hawachukui muda kwani hujikuta wakitolewa nje kutokana na matumizi yao makubwa kuliko kipato.
Sifa kubwa ya mfanyabiashara ambaye anasimama kama mchumi ni kuzijua hesabu zake kwa umakini jambo ambalo wasanii wetu wa kizazi kipya hawana.
Ukiachana na hilo, wengi wamekuwa wakitumiwa tu majina yao katika maduka lakini ukija kwenye ukweli, maduka huwa si yao, majina hayo hutumika kunufaisha biashara za watu na mwisho wa siku ukweli huja kubainika.
Upo mfano wa msanii mmoja aliyewahi kuwa na Baa maeneo ya Sinza, lakini ukweli ukaja kugundulika kwamba baa ilikuwa ni ya mwanamke aliyekuwa na uhusiano naye, pale walipoachana ndiyo siri ikavuja

No comments:

Post a Comment